
DIBAJI
Katika kitabu chake cha hadithi fupi, “Maskini Milionea”, Hamisi Babusa anaelezea bayana
kuwa, Afrika ni bara la fasihi simulizi. Hivyo wengi wetu tumeishi na kulelewa katika mazingira
ya kumegewa tanzu za fasihi simulizi k,v vitendawili,. Ngano, visasili, hekaya na hurafa.
Hadithi fupi ni hadithi zilizobuniwa na kuwasilishwa kwa lugha nadharia ya masimulizi.
Maneno haya yanaenda sawia na anavyoelezea mhakiki maarufu wa asili ya kiafrika, Abiola
Irele, kuwa hadithi fupi ni zao la utamaduni wa fasihi simulizi.
Hadithi fupi husimuliwa katika mtindo wa ploti ya moja kwa moja, tofauti na riwaya (novela),
ambayo husimuliwa kwa mitindo changamano.
Hadithi fupi husimulia kuhusu tukio moja tu linalotukia katika kipindi kifupi katika maisha ya
mhusika.
Hata hivyo, kuhusika kwa wahusika wachache ni sifa moja nyingine bainifu ya hadithi fupi. Hii
hutokana na kutokuwepo kwa muda wa kutosha wa kukuza wahusika wengi kama ilivyo katika
novela. Tujuavyo, wanadamu wana mazoea ya kusimuliana hadithi kila wanapotangamana na
jamii. Hivyo, hadithi zinazotufikia katika mfumo wa kitabu cha hadithi fupi kama mkusanyiko
huu wa “Siri ya moyo na Hadithi nyingine”, ni hazina kubwa inayokidhi utashi wetu wa kutamba
na kutambiwa hadithi.
Mkusanyiko huu wa matukio ni simulizi mbalimbali kwa njia ya fasihi andishi, inayoburudisha
na kuadilisha msomaji yule yeyote, na hivyo kuwa kama bibi na babu wa kutusimulia hadithi
kwa njia ya kitabu.
Ni jukumu kuu kwa wale wanaonzi kiswahili na maandishi ya Kiafrika kwa jumla kwamba, ili
waweze kupata uhondo uliomo ndani mwa fasihi andishi, ni sharti wawe na uzoefu wa
kuchambua na kubukua vitabu aina aina ili kujiweka katika muktadha wa misamiati, misemo,
vitendawili, misimu na ngano mara kwa mara na kumwezesha msomaji kukuza lugha kwa
mapana.
Wewe kama msomaji, unapopata fursa ya kupitia nakala hii ya hadithi fupi ya “Siri ya moyo na
hadithi nyingine”mwandishi Ally, ni ombi la mwandishi kwamba upate kuimarika, kumakinika
na kupata muda wa kutosha ili kwa kina uchambue kila sehemu pasi kusahau kumegea jirani
yako yale yote mazuri utakayokumbana nayo na kuzoazoa katika usomaji.
Shukrani za dhati kwako msomaji. Ni tumaini langu kuwa utaweza kukusanya mengi ya uadilifu,
uchochezi, ukosoaji na hata ya kulaani visa vingi vinavyotendeka miongoni mwa wanajamii
visivyo vya manufaa na elimu kwa kizazi kipya.
Endelea kukikuza Kiswahili. Endelea kuienzi lugha na pamoja twaboresha Kiswahili.
Wako mhariri,
Allan M. Ingutia.
AllyIM
March 28, 2020.

